Tuesday, May 23, 2006

SUALA LA KATIBA TANZANIA LITAZAMWE UPYA

Katika nchi yeyote duniani inayofuata misingi ya Kidemokrasia,Katiba ni chombo kinachotoa muongozo mkuu wa kuhakikisha Demokrasia inakuwepo nchini.Katiba ndio msingi wa Uongozi bora na muhimili wa Serikali,pia ndio muongozo wa Taifa,na mtetezi wa haki za binadamu Kitaifa na Kimataifa.
Nimesema suala la Katiba Tanzania litazamwe upya kwa sababu zifuatazo na za msingi:Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikilalamikiwa si na Viongozi wa vyama vya upinzani bali na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na watetezi wa Demoklasia. Suala la Katiba sio tu kwamba lilikuwa likiibuka kwenye vyombo vya habari tu bali hata kwenye vyomba vya sheria kama vile Mahakama kuu. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inasemekana kuwa na mapungufu mengi, na cha msingi zaidi ni kwamba Katiba hii ilitungwe\kuandikwa chini ya chama kimoja.

Katika mapungufu haya ya Katiba,Serikali imekuwa ikifanyia marekebisho. Marekebisho haya mimi nayaona kama kuichezea Katiba ya nchi,katika hili la marekebisho Serikali imekuwa inaamini na kuufanyia kazi msemo au methali ya usipoziba ufa utajenga ukuta, lakini wamekuwa wakishindwa kuelewa kuwa ufa huu ni mkubwa na umetokea kwa sababu nyumba hii imejengwa kwa matofali ya udongo,huku wao wakijaribu kuziba ufa huo kwa kutuma matofali ya sementi. Matokeo yake nyumba imelemewa na sasa inakaribia kuanguka yote, baada ya matofali ya sementi kuyazidi nguvu matofali ya udongo na msingi wake. Nini kifanyike kabla nyumba hii ijabomoka wakati wa kipindi cha masika?cha kufanya ni kuitisha mchango (mchakato) wa Kitaifa kuchangia nyumba mpya (Katiba mpya) itakayo jengwa pembeni au mbali kabisa na nyumba hii (Katiba hii) ya sasa.

Hapa kuna mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa mjadala huu wa kitaifa kuhusu katiba ya nchi,suala la msingi ni kutowaruhusu wanasiasa waichezee Katiba hii kwa kuongeza muda wao wa kukaa madarakani kama ambavyo tumezoea kusikia nchi mabalimbali za Africa zikifanya.Juzi Nageria wameshindwa kufanya hivyo.Uganda ilifanikiwa na kumuwezesha Museven kugombea tena, kwa kisingizio eti bado anapendwa na wananchi wa Uganda.Hapa ngoja niwafafanulie, viongozi wa Africa kuwa kupendwa kwao na wananchi hakutokani na mambo mema waliofanyiwa na viongozi wao, ila kunatokana na wananchi kuwaogopa viongozi wao pindi wakitoka madarakani wasije wakaanzisha fujo,Hali hii kisoikolojia tunaita nidhamu ya woga. Na nidhamu hii imeendelea katika nchi zitu za Afrika huku viongozi wakijivunia kupendwa na wananchi, wakisahau msemo wa kwenye Biblia wa kuzisoma Alama za nyakati na kuzielewa. Matokeo yake tumewaona viongozi wakijigamba kuwa wameleta na kuimarisha amani kwenye nchi zao. Kitu ambacho sio cha kweli huwezi kusema nchi yako ina imani wakati ndani ya nchi yako kuna wananchi wanaokufa kwa njaa au watakula nini mchana. Hivyo sio nchi ya amani ila ni nchi yenye wananchi waoga ambao wametulia kama maji kwenye mtungi ambao ukipata mtu wa kuutingisha mtungi huo huchukua muda kutulia.
Hii ni sawa na nchi zetu zile zinasemekana kuwa na amani,zikipata watu wachache wa kuwashawishi wananchi na kuanza vurugu au vita huchukua muda mrefu kupata amani mfano mzuri ni Ivory cost,Nchi iliyokuwa inachukuliwa kuwa nchi ya amani kule magharibi mwa Afrika,Angalia kwa sasa machafuko yalivyo. Na haya yanaweza kutokea Tanzania kama maoni ya wananchi na wadau mbalimbali wapenda amani na Demoklasia ya kutunga Katiba mpya ya nchi yatapuuzwa.

Mfano mzuri ni Zanzibar,tumeona na kusikia wanzibar kumi wameenda Mahakamani kudai hati ya mkataba wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika, sasa kama ungeitishwa mjadala wa Kitaifa kuhusu Katiba suala hili lisingeenda Mahakamani badala yake lingeongelewa na kujadiliwa na wananchi wa pande zote za Muungano Zanzibar na Tanganyika, mategemeo yangu kuwa matakwa au maelezo ya hawa watu wangeyapata kutoka kwa wananchi.
Nimesema suala la Katiba litazamwe upya kwa sababu nyingi tu ingawa nyingine nimeishazitaja lakini kuna nyingine. Katiba hii tuliyonayo inatoa mianya kwa Serikali zetu.zote mbili ya muungano na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.Kuichezeachezea au kuigombania kama mpira wa kona. Mwaka jana tuliona waziwazi uvunjaji wa Katiba hii pale Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipoamua kuwa na Bendera yao, ambayo mpaka sasa hivi inatumika Kimataifa, Hapa kwenye michezo, tumeiona Bendera hiyo ikibebwa na Timu ya Polisi Zanzibar. Hapa ndio tunaweza kuanza kusema sasa Tanzania Visiwani ina uhuru wa Bendera,kama sio hivyo basi tukubali na kukili kuwa Zanzibar kuwa na Bendera yake ni uvunjaji wa Katiba.
Nasema haya yote kwa masikitiko na kwa mshangao kwa sababu kipindi chote cha miaka 40 ya Muungano hakuna aliyetegemea au kutarajia tukio kama hili la Bendera ya Zanzibar, wote tuliamini kuwa Bendera zote za Zanzibar na Tanganyika zilizikwa mnomo 26\4\1964. Tangia hapo tumekuwa tukiamini kuwa Tanzania ni nchi moja na ni Jamuhuri ya Muungano.Angalia Katiba ya nchi Ibada ya kwanza naya pili “ Tunaposema Jamuhuri ya Muungano, Tunaimarisha eneo lote la Tanzania bara na la Tanzania Visiwani. “Hivi Zanzibar ikiamua kuwa na wimbo wake kuna mtu atahoji?Au akitokea kikundi cha watu au mtu akadai kuwa na Bendera ya Tanganyika kwa kutumia vigezo vilivyotumiwa na Serikali ya Zanzibar kuwa na Bendera yake tutasemaje? Au tutaenda Mahakamani au hicho kikundi tutakiweka kizuizini. Kama Zanzibar imekuwa na Bendera yake iko wapi Bendera ya Tanganyika? Na itakuwa wapi Bendera ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania?
Siku chache zilizopita Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kutaka baadhi ya vifungu kwenye Katiba vifutwe,ikidai mhimili huo wa dola umepewa mamlaka hayo Kikatiba. Sasa nashangaa kama Katiba ndio yenye mamlaka makubwa kwenye nchi je Mahakama itakuwaje na uwezo wa kufuta baadhi ya vipengele kwenye Katiba, kama Katiba ndio mama wa Taifa. Mtoto wa mama huyu hamkosoe mama yake hadharani au aseme mama anamakosa kabla ya mme wake (Serikali na wananchi) ajaona hayo makosa. Au labda mme wake ameyaona ila kwa sababu mke wake ni mzuri anaogopa kumkemea.Uamuzi wa Mahakama kuu wa kuagiza kufutwa kipengele kinachowalazimisha watu kugombea nafasi za uongozi kwa kupitia nyama vya siasa. Na kuagiza kila mtu aruhusiwe kugombea nafasi za Uongozi kwa kupitia chama chochote, Mahakama kuu katika maamuzi yake imeamua kuwa ni haki ya kimsingi naya kila raia kugombea Uongozi ndani ya nchi bila kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha Kisiasa. Mahakama kuu imetoa ukumu hii kulingana na haki za binadamu na kutokana na Katiba hiyohiyo,Inayokatazwa kuwepo kifungu chochote ndani ya Katiba kinachopokonya haki mwananchi iliyo katika Katiba.
Inaonekana hukumu hii ya Mahakama utaadhiri sheria nyinginezo, sasa ili kulizuia jambo la msingi ni kuhitishwa mjadala wa Taifa nchi nzima badala ya Serikali kukimbilia kukata rufaa kwa sababu kama Katiba imeipa uamuzi huo kwa kuzingatia Ibara ya 30 kifungua cha 3 kinachosema: Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika sehemu hii ya sura hii au katika sheria yeyote inayohusu haki yake au wajibu wake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea ilitavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano anaweza kufungua shauri katika Mahakama kuu. “sasa kwa msingi huu ni bora suala hili la Katiba ya Jamhuri ya Muungano litazamwe upya na wadau wote wenye mamlaka ya kufanya hivyo chini ya Katiba.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home