Tuesday, March 28, 2006

KWENYE HILI NANI ALAUMIWE?

Nilipuko Darasa la sita katika shule ya msingi ya Karwoshe kata ya katoma, Wilaya ya Bukoba , mwalimu wangu wa Kiswahili alitufundisha wimbo ambao mpaka sasa bado naukumbuka na baadhi ya Beti za wimbo huo ni hizi:

Tanzania Tanzania, nakupenda Kwa moyo wote
Nchi yangu Tanzania, Jina lako Ni tamu sana
Nilalapo nakuota wewe niamkapo Ni heri mama we,
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote

Nchi yangu Tanzania, ninapokwenda safarini
Kutazama maajabu biashara nayo makazi
Sitaweza kusahau mimi, mambo mema ya kwetu kabisa
Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote.

Tanzania watu wengi wanakusifu
Siasa yako na desturi, vilituletea uhuru
Sitaweza kusahau mimi mambo mema ya kwetu kabisa
Tanzania Tanzania nakupeda kwa moyo wote.

Shairi hili linajieleza lenyewe, kwamba lilitungwa na mtu mwenye mapenzi na Tanzania . Mtunzi anasifia sifa mbali mbali ilizokuwa nazo Tanzania ya kipindi hicho,wakati mtunzi akiitukuza Tanzania , Mtunzi anajiwekea ahadi kwamba hataweza kusahau mambo mema ya Tanzania, anafikia hatua ya kuota Taifa la Tanzania pindi alalapo na ahamkapo ni heli kwake.
Nikikumbuka Jinsi tulivyokuwa tunaimba wimbo huu, huku tukijivunia nchi yetu, mimi kama Mtanzania nilijisikia kuwa mmojawapo kati ya watu wenye bahati kubwa duniani, kwani nilikuwa naona na ninafikiri nikiwa nchini hata nikiwa mkubwa mambo yataendelea kuwa ya heli. Lakini kabla sijakaa sawa mambo yakaanza kubadilika ghafla, nasema gafla, kwa sababu imekuwa mapema mno kufanya mabadiliko ya haraka kutoka ujamaa, ambao ndo ulileta hiyo heli anayoiota mtunzi wa shairi, hadi utandawazi ambao umeondoa heli hiyo. Na matokeo yake Tanzania imeanza kubadilika kutoka kisiwa cha amani hadi kisiwa cha majambazi.
Nasema Tanzania kutoka kisiwa cha amani hadi kisiwa cha majambazi sio kwenda watanzania wote ni majambazi la asha, ila napenda niweke wazi kuwa ujambazi nchini umezidi na unatisha. Nampongeza Mh. Rais Jakaya Kikwete kwa kuliona hilo na kuanza kulivalia njuga lakini je tujiulize watendaji wengine walioko serikalini nao wana moyo huu kama wa Rais?
Mtu atakubaliana na mimi kuwa wakati Rais anapambana na Rushwa, ujambazi, ujinga na ubadhilifu wa mali ya huma. Viongozi wengine serikalini wanaona kuwa ni kero na wanadhani Mheshimiwa Rais amewasaliti kwa kuwageukia wao, sasa wanachokifanya ni kuanza wao kwa wao kulindana, huu nao ni ujambazi. Hasa ujambazi mkubwa, kuliko tunavyofikiria.
Na ujambazi huu umechukua kasi baada ya kuanza ubinafsishaji, ambao umegeuza mali ya umma kuwa mali ya mtu mmoja au watu wachache, kwa manufaa yao, kuliko manufaa ya jamii nzima.
Nimegusia suala la Ujambazi, Ujambazi huu uko mara mbili kuna ujambazi unaofanywa na vijana walioshindwa maisha au wenye uchu wa pesa, wanaotumia msemo wa “ponda mali kifo chaja” au ukipata wakati tumia wakati. Ujambazi mwingine ni hule wa ubadhilifu wa mali ya umma na rushwa unaofanywa na viongozi wa serikali walioko madarakani na katika mashirika mbalimbali ya umma. Napenda nirudie sio viongozi wote ni majambazi au vijana wote ni majambazi;
Swali linakuja kwa nini vijana wengi sasa hivi, wajiingize kwenye wimbi la ujambazi? Jibu ni kwamba siasa za Tanzania za sasa zimewafanya hivyo. Na hii ni baada ya
(Sovereignty) ya Tanzania naya vijana kuthibitiwa na matakwa ya wafadhili.
Leo hii vijana wamegeuzwa kuwa manamba wa matajiri, chinga wa Dar, nyoka wa Mererani, wapagani wa Kariakoo, vibarua wa maofisini na mashambani. Kinachotokea katika Tanzania ya sasa ni uzao au matunda ya mbegu zilizopandwa na viongozi wetu ambao wanatumia ufisadi na mbinu chafu, ili wanufaike na mfumo wa kiuchumi uliopo huku wakijitahidi kuumiza akili za vijana na kuwafidi kwa kila hali. Vijana wamefikia hatua ya kutokuwa na matumaini mbele ya jamii wanamoishi. Uku wakiambiwa vijana ni Taifa la kesho.
Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq katika kitabu chake “The Revolution and the Youth” anasema kwa sababu vijana wanamaisha marefu ya kuishi, wananafasi nzuri ya kusimamia na kuongoza mapinduzi, hapana budi wapewe mazingira mazuri na uwezo wa kusimamia mazingira mazuri na uwezo wa kusimamia mapinduzi”. Lakini kwa Tanzania wamepewa mazingira hayo? Mtu atakubaliana na mimi kuwa mazingira hayo kwa kijana wa Tanzania hayapo, tunachokiona ni maendeleo ya kitabaka ya kiuchumi na kijamii kuwa utukufu wa soko, viongozi kuendelea kulindana, kudai na kutetea haki kuwa ugaidi, uvamizi wa mali ya Taifa kuwa uwekezaji, waheshimiwa wetu Bungeni kudai kuongezewa mshahara na marupurupu mambo haya yote yanatosha kuwa chanzo cha ujambazi kwa vijana.
Napenda niwe wazi kuwa huwezi kutofautisha rushwa, utandawazi,ubadhilifu wa mali ya humma, na ujambazi.Hivyo vyote vinakwenda sambamba, ndo maana ninasema kwamba kuna ujambazi unaofanywa na viongozi wa serikali walioko madarakani, sio wote lakini nisije nikaeleweka vibaya .Mwalimu Julius Nyerere aliwaambia wananchi wa Shinyanga katika moja ya mikutano yake kuwa “Nyie wasukuma ni matajiri wakubwa kuliko makabila mengine kwa sababu nyinyi mna pamba ya aina mbili mna pamba ya chini na pamba ya juu,lakini kalime kwanza Pamba ya juu, ikiisha kalime ya chini” lakini wakati wanalima pamba ya juu, wakaja matajiri wakubwa (makampuni ya kigeni) ambao kwa watu wengi wa Shinyanga wanawaona kama majambazi, wakaanza kulima pamba ya chini (dhahabu).Hawa wanaonekana ni majambazi kwa wananchi kwa sababu faida yake hawaioni matokeo yake inawanufaisha viongozi wa serikali walioko Dar. Na matajiri hao ambao wanapeleka mapato nje ya nchi.
Ebu jiulize kama TANAPA ina kitengo cha ujirani mwema, kinachotoa asilimia ya mapato ya utalii na matunda yake kwa wananchi wanao zunguka au kuzungukwa na hifadhi hizo, ili yawanufaisha wenyeji, kwa nini isifanyike kwa wasukuma walioambiwa walime pamba ya juu kwanza? Freman Mbowe alilizungumzia suala hilo likaonekana kuwa anataka kuleta dhana ya ukanda, sasa mbona TANAPA hawalalamikiwi kwa kufanya hivyo au huo sio ukanda. Ebu jiulize tena kama kweli msukuma wa Shinyanga wa leo atakuwa akijivunia kuimba wimbo wa “Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote” na kwa nini kijana wa maeneo kama hayo asiwe jambazi? Ebu fikiria, tunapopambana na ujambazi tukaacha chanzo cha ujambazi, nani alaumiwe kwa hilo? Juzi wamachinga Mwanza na Dar. Walibomolewa vibanda vyao na kukatazwa kuuza bidhaa zao mitahani, sasa je tumewajengea mazingira yapi vijana hawa, kama sio ujambazi. Nampongeza Waziri Mkuu kwa busara zake aliweza kuliona hilo. Sasa ni zamu ya kupambana na viongozi na sio wafanyabiashara tu, ni wakati wa kupambana na wawekezaji, wanaoiba mali ya umma bila wananchi kunufaika.
Wananchi waliwataja polisi wanaoshirikiana na wezi hatujaona hatua zilizochukuliwa matokeo yake tukaona makamanda wanaamishwa vituo vyao vya kazi, lakini nayo hiyo ni hatua ngoja tuone,sisi tunaiunga mkono serikali yetu.
Ebu jiulize kama kweli muhandisi wa Wilaya ya Ilala alikuwa makini kiasi gain kuruhusu ujenzi wa Village Hotel iliyouwa watu zaidi ya mmoja uendelee, wakati anajua kabisa kuwa jengo hilo halina kibali cha kuendelea kujengwa huo kama sio ujambazi ni nini? Nalo nani alaumiwe?
Napenda nimalizie kwa kusisitizia kwamba uwezi kutofautisha rushwa, utandawazi, ubadhilifu wa mali ya umma na ujambazi.Na kama alivyosema Rais wa zamani wa Africa ya Kusini mzee Nelson Mandela kuwa “kama msomi kunyamaza kimya katika mambo ambayo si mazuri kwa jamii, elimu yako haitakuwa na manufaa tena kwa jamii, na unastahili kutupwa jela kwa kosa la jinai ambalo ni kubwa kuliko kosa la uhani” na mimi ninasema kuliko kukaa kimya, bora ni seme si lazima mabadiliko yawepo hata Mungu aliwambia manabii kuwa si lazima watu wabadilike lakini wakae wanajua kuwa nabii alikuwepo. Na mimi nasema ni nani halaumiwe? Tanzania Tanzania jina lako ni Tamu sana nilalapo nakuota wewe lakini niamkapo sio heli tena.

1 Comments:

At 2:47 AM, Blogger Marcu said...

Hello !
I'm a french man and i love the song :"Tanzania Tanzania, nakupenda Kwa moyo wote....."
I'd like to heard it and get it but I don't find it on the web, can you help me, maybe sand it to me by internet ? It will make me so happy ! Thank you very much if you answer to me !

 

Post a Comment

<< Home