Wednesday, January 11, 2006

UMASKINI WETU NANI ALAUMIWE?

Je kuna njia ya Mkato katika Maendeleo ya Kiuchumi ya Tanzania?. Swali hili limezua mjadala mkubwa kwa miongo mingi. Mjadala huu umewaingiza wahazili wa vyuo, wachumi wa kimataifa, umoja wa Mataifa na Vitengo vyake vya uchumi, Umoja wa Africa ( Au), wanazuo na viongozi wa dini. Maazimio mengi yamewekwa , Ripoti mbalimbali zimewekwa. Matokeo yake yamekuwa ni sawa na bure, Huku nchi za Africa, Tanzania ikiwa ni miongoni zimebakia kuwa maskini wa kutupwa cha kutisha zaidi hali inaendelea kuwa ngumu.
Mpaka sasa maswali mengi ya kiuchumi bado hayajajibiwa, ingawa tunaambiwa uchumi wa nchi unakua. Je tutaendelea kupokea maelezo hayohayo au kuna njia nyingine? Au tuendelee kuziona nchi za magharibi kama Mungu wa pili? Kwa sababu wakati Watanzania tunazidi kulia na kupigana na umasikini, Nchi za magharibi zinazidi kung’ara machoni mwa watanzania kuanzia kwa viongozi mpaka kwa mwananchi wa kawaida. Na sasa tunawaona kama watu wema, wa mcha Mungu wanaosamehe watu madeni yao, wanaotoa msaada wa nguo kwa masikini, watu wanaowaangalia watoto yatima na wajane, watu wanaopenda maendeleo ya Watanzania, watu waliotuletea demokrasia na sifa nyinginyingi tu ambazo mpambe wa mwenye Mgodi Mererani angependa amsifie bosi wake pindi shimo lake likitoa madini. Matokeo yake ni watanzania kuendelea kuchezea matapishi yetu wenyewe.
Ebujiulize lipi limeenda kombo? Je ni urithi tuliorithi kwa maendeleo hafifu au viongozi wetu? Waza maswali mengi tu ujiulize na kwanini sisi na siyo wao? Slogan mbalimbali zimetawala medali za siasa na uchumi kama “saa ya ukombozi ni sasa” Ujamaa na kujitegemea “Haki sawa kwa wote:” Mageuzi na umoja “ Uchumi wa soko huria” Yako wapi matokeo yake kwa mwananchi wa kawaida?
Hebu tujiulize tutaendelea na majaribio haya au ndiyo tunajaribu njia nyingine ya mkato? Hili ni swali ambalo kila mtanzania anapaswa kujiuliza, nasema kila mtanzania ajiulize kwasababu Maendeleo ya Kiuchumi au Kisiasa hayataletwa na mtu mmoja, ni ya watanzania wote kwa pamoja. Baba wa Taifa hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kwamba “ aliwapeleka wamasai shuleni kwa FFU, waliporudi nyumbani wakati wa likizo, hakuna aliyerudi shuleni tena” hayo yalikuwa ya wamasai sasa tunaendelea kushuhudia kabila la wahazabe wakikataa kutoka porini lakini viongozi hilo hawalizungumzii. Chakushangaza tumezidi kukaa kimya wakati watoto wa kike wakiendelea kutahiriwa ili kuwaongezea soko la ndoa , Jamii ya watoto yatima ikibaguliwa, wajane wakinyang’anywa mali walizochuma na Waume zao enzi za uhai wao,tukizidi kuwanyanyapaa wagonjwa wa ukimwi. Maofisini nako Ugonjwa wa njoo kesho na rushwa vikikosa tiba na kuendelea kuwa kero kwa Mtanzania, Kufungua Kampuni kwa Mtanzania huchukua siku mia ishirini na tisa (129) wakati kwa mgeni ni siku ishirini na tisa ( 29 ) Kazi maofisini hupatikana kwa vigezo vya kumfahamu mtu na si mtu anajua nini . Uporaji wa mali ya nchi kuitwa uwekezaji , cha kushangaza hawa wawekezaji wameingia mpaka kwenye biashara ambazo watanzania wanaziweza.
Leo hii nenda Kariakoo utawakuta wachina wana maduka ya nguo za mtumba, maduka ya vyombo vya jikoni,jiulize wapemba na wachaga hawapo wakuendesha hayo maduka, nasikia eti kuna wawekezaji kwenye kuuza karanga pembeni mwa barabara kutoka nje ya nchi. Ili kufahamu ya leo lazima utazame ya nyuma na kufahamu ya mbele lazima tuangalie ya nyuma na ya leo, hii ni kwa njia ya kisayansi.Tunaambiwa umaskini wetu umesababishwa na umaskini wetu,falsafa ya mmarekani mmoja ya “vicious circle of poverty”kulifunga duara hili kufuatana na maelezo yake tunahitaji wawekezaji wa nje{foreign investment}Wakati ni sahihi kuwa uwekezaji huo ndio umetufanya tuwe maskini.
Wanafalsafa wanaamini kuwa hakuna kinachotokea katika maisha ya binadamu leo ambacho ni kipya.Wanaamini kuwa kila kinachotokea leo ama kimeandikwa kwenye misaafu mbalimbali ya dini au kilitabiriwa na mababu zetu miongo kadhaa iliyopita.
Hebu tujiulize hatuko maskini sasa kwa sababu ya ukoloni?kwa njia moja au nyingine tumetawaliwa na bado tunaendelea kutawaliwa kifikra mpaka leo{ukoloni mamboleo}.Si ukoloni uleule ulioleta uwekezaji wa nje?mbona bado tuko maskini?Jiulize itakuwaje leo utukomboe kutoka kwenye umaskini?Ni kweli na itaendelea kuwa kweli kwamba uwekezaji wa nje hauwezi kutusaidia kujikwamua na umasikini kwa misingi ya kila mwananchi kunufaika, Kwa mtindo huu wa makampuni haya kuchukua faida kubwa nje ya nchi. Matokeo yake ni pengo la wenye nacho nawalala hoi kuzidi kuongezeka kwa kasi ya kutisha kila kukicha. Huku sera zetu zingiendelea kusisitiza uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ( Soko la dunia ) au soko huria ambalo mnunuzi ndiye anayepanga bei na si muuzaji. Tunavyozidi kuzalisha kwa ajili ya soko hilo, (soko la dunia) ndivyo tunavyozidi kusahau au kupiga kumbo uzalishaji kwa ajili ya watu wetu na maendeleo yao.
Chukua mfano wa nchi za Korea ya kaskazini, Botswana, China, na Albania hizi nchi zote zilikuwa maskini kama sisi lakini wao waliamua kuachana na Mfumo wa Bank ya Dunia, IMF, na soko la dunia kwa kufuata uchumi wa kijamii wa Kuzalisha kwa ajili ya watu wao na maendeleo yao ya kiuchumi , matokeo yake mataifa ya nje yamewafuata ili wawauzie bidhaa zao kwa bei inayopangwa na muuzaji na sio bei ya mnunuzi.
Jiulize tena na tena umasikini wetu nani alaumiwe? Kwa kuuliza swali kwa njia hii ni rahisi kuona kwa kupitia kwenye kioo, kipi kilichosababisha tuwe masikini wakati nchi ni tajiri?Ingawa nimeandika sintashangaa kusikia mtu au kundi la watu wenye msimamo wa soko huria ,soko la dunia na muongozo wa Benki ya dunia,wakinibeza,kwa kuuliza swali hilo,kwa sababu mafundisho na maelekezo yao yanamuangalia mtu au kundi la namna ya kwangu kama mtenda maovu na Adui wa umma.Ebu endelea kujiuliza kama Mmarekani au mwingereza anayekaa New York au London kupanga maendeleo ya Mtwara au Lindi?Ambako hajawahi kufika.Jiulize tena na tena .
Nina matarajio mengi kutoka katika serekali ya awamu ya nne ya mheshimiwa Jakaya Kikwete.Mheshimiwa Rais anaonekana kuwa ni mtu wa watu na mpenda maendeleo ya watanzania walio wengi.Nasema hayo kwa sababu ni kiongozi wanchi ambaye watoto wake wamesomea na wanasomea Tanzania.Huo ni mfano mzuri wa kuigwa na viongozi wengine, na hii inaonyesha ni jinsi gani mheshimiwa Rais alivyo na imani na elimu ya kitanzania inayomfundisha mtanzania kuwa mtanzania kila sehemu alipo. Hotuba yake ya bungeni inaongeza matumaini yangu kwa kweli. Na kumuona kama mtu anayeweza kubadilisha mkondo wa uzalishaji kutoka kuzalisha kwa ajili ya soko la dunia kwenda katika uzalishaji kwa ajili ya wananchi, kubadilisha sera za uwekezaji kutoka kutegemea uwekezaji wa nje kwenda katika uwekezaji wa ndani. Wakati huhuo na sisi wananchi tuwe tayari kumuunga mkono kwani maendeleo yetu hayataletwa na Rais tu bali na sisi wanachi tuwe tayari kubadilika.
Wakati wa ukombozi ni huu tusisubiri mtu wa kupeleka watoto shule kwa FFU ni jukumu letu sisi wote kufanya kazi kwa Ari mpya, Kasi mpya na nguvu mpya. Je tunao uwezo wa kufanya maamuzi yetu wenyewe? Kama tunao Mungu Ibariki Tanzania ,Mungu mbariki Mheshimiwa Jakaya Kikwete.

9 Comments:

At 7:42 AM, Blogger boniphace said...

Hongera karibu sana hii makala safi sana nakubaliana na vipande vingi vya juu na pia kujenga shaka katika hitimisho la makala hii. Tuombe maana huu mjadala wa awamu ya nne unatanuka sana na huko Tanzania nasikia ni dhambi kuzungumza upande wa pili wa shilingi wa serikali tukufu ya wananchi lakini kwa walio ughaibuni wameshaona na hawaogopi kutamka kuwa twendako hatukuoni maana makosa yanaanza mapema mno.

 
At 12:08 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Karibu sana uwanjani,makala yako imesimama wima na uliyoyasema yana mantiki kubwa.Karibu sana

 
At 12:41 AM, Blogger Fikrathabiti said...

Karibu brother kwenye ulingo wa kifikra uweze kutoa yako ya kumoyo yaliyojikita zaidi katika kufichua uzandiki uliowajaa viongozi wa nchi yetu.
Nipo zanzibar ila masomo yangu ya stashahada ya uzamili nayafanyia hapo ESAMI Arusha,na ninatarajia kuja mwezi huu mwishoni kwahiyo tutaweza onana katika kubadilishana changamoto kadha wa kadha.
ALUTA CONTINUE:

 
At 2:11 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Ishaalah!Nadhani sasa naweza kuwa na mtu "Muburogu" wa kumtembelea ana kwa ana, tukabadilishana hili na lile, hapa hapa Arusha!
Nimefuarahi kuzidi maelezo. Wakati wa ukombozi ni sasa, tusingoje kesho...ni kweli.

 
At 2:15 AM, Blogger Fikrathabiti said...

Mr Ndyemalila asalam aleikun!
E-mail address yangu ni ismaelmat@yahoo.com nakuja tar 30 january huko meru,kwahiyo twaweza onana tukijaaliwa.

 
At 11:13 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Umeingia kwa nguvu nasi tunakukaribisha kwa nguvu. Kuna umetoa takwimu zimenifurahisha sana: mtanzania kuanzisha kampuni anatumia siku 129 (kutokana na njoo kesho na rushwa), mgeni tunayemwabudu anatumia siku 29. Chini ya mwezi mmoja. Pia suala la wapanga maendeleo ya Mtwara kuishi Marekani au Ulaya. Ndio kichekesho cha dunia hii inayoendeshwa na kundi dogo la wanaume wa kizungu wakisaidiana na vibaraka wanaofanana nasi.

Nitafurahi nikisikia kuwa wanablogu hapo Arusha mmeweza kukutana ana kwa ana. Jeff na Boniphace walikutana karibuni.

 
At 1:30 AM, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

karibu sana bwana Ludovick. huu ni uwanja bora kabisa wa kukuweka huru na kufahamu mnyambuliko wa uhuru kwa pande zote pia. ni njia sahihi kabisa ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru!

ninakubaliana kabisa na wewe kuwa na mara nyingi kilio changu ni kuwa maendeleo yetu watanzania yamekamatwa - arrested development. mfano hiyo data uliyomwaga kuhusu kufungua kashughuli kwa mzawa. nilisikia kwa Tv juzi wanasema SA ni inchi ya 21 ulimwenguni kwa mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza. ninaendelea kumfuatilia Raisi wetu kwa ukaribu zaidi lakini dalili za awali zinaonyesha anaweza kuwa kiongozi maarufu wa watanzania, pengine kuliko hata mwalimu.

 
At 5:28 AM, Blogger mloyi said...

Moto mwingine huu hapa! Makala safi iliyochambuliwa kikwelikweli, inaingia kwenye familia ya mburogu. Tunasubiri makala nyingine zenye habari za kuelimisha na kutujenga zaidi.
Nafasi iwazi kwa mchango wako. Karibu.

 
At 3:27 AM, Blogger Indya Nkya said...

Kaka ntakuwa mchoyo wa fadhila kama nisiposifia hii makala na kukukaribisha

 

Post a Comment

<< Home