Thursday, May 04, 2006

YUPI KIONGOZI BORA WA UMMA?

Katika nyanja hii ya uongozi kuna kiongozi bora,mwaminifu kutoka kwa watu ambaye yuko tayari kufanya kai kwa manufaa ya umma. Na ubora huo wa uongozi sio huo wa kuongea tu, bali ni wa vitendo. Kiongozi wa umma ni yule anayetumia busara na upeo alivyopewa na mwenyezi Mungu kuwashauri na kuwasaidia watu kuelewa matatizo yao pamoja na sera za maendeleo, kwa kutumia Hoja za kimsingi. Watanzania wa leo si watu wakupewa Takrima.,Bakishishi, au sherehe, Hawapendi propaganda na ahadi kubwa zisizotekelezeka na Hawapendi kusikiliza viongozi wao wakilumbana na kutupiana lawama kuhusu matatizo yanayoikumba jamii.

Viongozi wa umma na hii ikijumuisha kila kiongozi lazima aonyeshe kufanya kazi kwa vitendo na kwa maneno. Wakati mwingine lazima tukumbuke kuwa kiongozi hawezi kufanya kila kitu kwa watu wake. Kiongozi anaweza kutoa muongozo mwelekeo au dira na jinsi gani watu waendeshe nchi yao wenyewe.Kiongozi wa umma hapaswi kuwa anatoa haadi ambazo hazitekelezeki au kukaa na kuanza kulaumiana lazima kiongozi anayeelewa matatizo waliyonayo Watanzania na atoe muelekeo na Muongozo ulio bora kwao ili waondokane na haya matatizo.

Hili ni jambo la muhimu, Kiongozi lazima aelewe na kufahamu ukweli wa matatizo tuliyonayo na aonyeshe kwa umma, kwa kutumia Nguvu zake ni jinsi gain Tanzania ya leo itaweza kuondokana na umasikini huu na kuwa nchi yenye neema. Kiongozi kama kiongozi haina maana kujidanganya kwa jambo Fulani Hasa umasikini kuwa haupo au kiongozi kujisifu mbele ya wapiga kura eti amepandisha bei ya kahawa, pamba., korosho nk. Kiongozi lazima aelewe kuwa matatizo yetu hayawezi kuisha kwa kujifanya na kuamini kuwa hayapo au kwa sababu tunawalaumu watu Fulani kuwa chanzo cha matatizo.

Viongozi lazima waelewe kuwa Hawawezi kuendesha nchi kwa kulalamika lalamika kuwa sisi ni maskini au Bei ya kahawa imeshuka, haisaidii ni sawa na kulalamika kuwa mvua haikunyesha. Kiongozi bora lazima ajue kuzitambua na kuzielewa alama za nyakati hizi, hata kama ziko nje ya uwezo wake, lazima ajue ni jinsi gain ya kuyatatua matatizo yanayotokea au kujitokeza nyakati hizi.Kiongozxi lazima ahaakikishe mipango ya Taifa inatekelezwa kwa kutumia akili aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hakuna njia nyingine, wala hakuna njia ya mkato.

Watanzania ni masikini na huu ndo ukweli wa mambo. Na ni tabia ya mwanadamu yeyote kuona utajiri na bahati alivyonavyo mwenzake kuliko yeye. Haipaswi kuwa kazi ya Kiongozi wa Tanzania kuwarubuni na kuwashawishi watu kuchukiana wao kwa wao kwa kisingizio za mali walizonazo. Wakati huo huo lazima ieleweke kwa umma na viongozi wetu kuwa Hakuna kiongozi anayepaswa kutumia madaraka yake vibaya ili kujipatia mali.



Kiongozi lazima afahamu kila kipato anachopata lazima kipatikane kihalali kama malipo yake kuto kwa umma, kwa kazi anayoifanya. Hii haitoshi kiongozi lazima aonyeshe ni jinsi gain ya kuendeleza nchi na watu wake. Mfano kama wawindaji kumi waliokamata sungura mmoja itakuwa ni ujinga na upotezaji wa muda kama watasitisha uwindaji. Na kuanza kugombania mgawanyo wa nyama wa sungura huyo mmoja. Lakini watakuwa wanafanya vizuri na Busara kama watatafuta mbinu na njia mpya za uwindaji ili kujiongezea wingi wa nyama, Na hii ni sawa na Viongozi wa Tanzania. Hii ni nchi Masikini, nchi isiyozaa matunda ya kumtosheleza kila Mtanzania ili aishi maisha bora , Tunafanana na wawindaji kumi wenye sungura mmoja katikati yao, hatuna njia ya kuondikana hili .Hii aina maana kuwa serikali iongeze pesa nyingi kwenye mzunguko wa uchumi . Kama kiongozi mmoja wa chama cha siasa aliyekuwa anatumia falsafa ya kuwajaza watu mapesa . Kuongeza fedha nyingi kwenye uchumi wa nchi ni kuongeza mfumuko wa bei kwenye nchi jambo ambalo litaharibu uchumi wetu na hili ni bora kila kiongozi akalielewa.

Haina maana kiongiozi kuelewa Takwimu kabla Hajatambua kuwa Tanzania ni masikini . Tena ya kutupwa. Tunaona na tunaishi na umasikini , wakati mwingine viongozi uchanganya mambo kwa kutazama watu wachache wanaoendesha magari yao binafsi au kwa takwimu zinazotolewa na waziri wa fedha wakati wa kipindi cha Bajeti Bungeni, na kuamini kuwa nchi yao ni tajiri na kwamba umasikini tulionao ni kutokana na mgawanyo mbaya w rasilimali au ni unyonyaji,wakati mwingine kuamini kuwa umasikini hamna kabisa, kama kiongozi mmoja wa juu kwenye Serikali ya awamu ya tatu aliyesema hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kukosa kupata shs 500/= kwa siku. Sina maoni kuwa mgawanyo wa utajiri wa nchi hauna maana la asha, una maana sana Hasa kwa watu kama sisi tunaamini na kukubali azimio la Arusha kuwa lazima pawepo na mgawanyo sawa wa mali ya umma. Ni sawa na wale wawindaji kumi wenye sungura mmoja katikati yao, lazima tutafute njia ya kuongeza pato la taifa sisi wenyewe tukitaka haya yote yatimie, lazima tusimamishe upandishaji wa mishahara ya vigogo serikalini na tuongeze mishahara ya wafanyakazi wa kima cha chini.

Lazima tuimarishe vyama vya ushirika ili kupunguza unyonyaji wa madalali kwa mkulima mdogo , ni lazima tutafute njia mbadala na mfumo mpya wa kilimo tuondokane na kilimo cha Jembe la mkono tuamie kwenye matumizi ya trekta , lazima serikali ipambane na makampuni yananyotengeneza na kuwauzia wakulima mbegu zisizofaa serikali lazima iongeze ruzuku kwenye pembejeo za kilimo.
Kila kiongozi lazima aelewe kuwa watanzania walio wengi wataendelea kuishi vijijini,mahitaji na maisha yao yote yatategemea kilimo. Hii ina maana kuwa lazima kilimo chetu kiwe cha kisasa na ni lazima tuimarishe vyama vya ushirika ili kuwawezesha wakulima wetu wawe na akiba kidogo ya kuhifadhi, na ni jukumu la serikali kuakikisha kuwa inawasogezea wakulima hawa Benki karibu. Tukiwasogezea Benki karibu wakulima Hawa kama vimebaki vihela vyao, hivyo vlivyosalia bada ya kununua vitu dukani au labda baada ya kununua Ngo’mbe au ameongeza mke wa pili na bado kuna kaakiba kadogo , kama Benki iko karibu anaweza kuviweka vipesa vyake hivyo akiba.Mkulima akiweka akiba yake Benk anachohitaji ni usalama tu wa vile vihela yvake, Hatafuti kuzaa. Kila kiongozi wa umma lazima hayo hayafahamu.

Na mimi nayataja hivyo ili kusudi viongozi wa serikali ambao wanaamini na kusadiki ushauri unaotolewa na Benk ya Dunia na mashirika yake, na wale wanaoamini kuwa uchumi wanchi utayumba kwa sababu kiongozi au viongozi wa Umma watakataa masharti mazuri ya mashirika hayo, sio kweli.Mashirika haya ya Kimataifa yanapotosha na kutuyumbisha, lazima viongozi wetu mkatae, naeleza makusudi muelewe mambo mengi ya mashirika haya ya Kimataifa (IMF na wenzake). Hayana chembe ya utaalamu ndani yake, ni udanganyifu mkubwa. Ebu fikiria ni kiongozi gani wa Benk ya Dunia aliyewahi kufika Singida au Kigoma na kuweza kuyaona matatizo ya wananchi wa Mikoa hii angalau ata kwa dakika tano tu. Jiulize maendeleo ya Ulaya au nchi zote za magharibi yametokana na mashirika haya? Nasema ili kila kiongozi mwenye uchu wa maendeleo ya Mtanzania ajue. Kuwa haina maana, kwamba kabla hatujapandisha bei ya umeme twende kuyaomba mashirika haya yaturuhusu na ina maana kuwa mipango yetu ipitie kwenye mashirika haya; nakataa kata kata.

Mashirika haya na vibaraka wa mashirika haya wanaamini kuwa nchi inaweza kuendelea na kumiliki maendeleo yake bila wananchi wake kumiliki njia na mchakato mzima wa uzalishaji mali wakati duniani kote na katika vitabu vya uchumi, nani anamiliki nini ni swali na suala la msingi kwenye nchi husika. Uku mashirika haya yakiendelea kutupotosha, viongozi wetu na wananchi tunazidi kuonyesha.“qui tacet concentive viditur” kimya means ndiyo au tunakubaliana nayo.

Katika mchakato mzima wa kuonyesha na kuelekeza ni yupi kiongozi wa Umma, na ni mkondo gani Taifa lifuate. Sijawasahau waandishi au watu wenye taaluma ya habari bila kuwasahau wanaomiliki vyombo vya habari, kwanza kabisa nawapongeza sna kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha, na kuburudisha jamii ya Tanzania ambayo ni maskini. Make nisipowapongeza nitakuwa mchoyo wa pongezi kama wahaya wanavyosema “Entasima Ekalya omutima gyemanzi”

Tanzania tumepiga hatua kwenye uhuru wa vyombo vya habari.Lakini najiuliza Je uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa kubomoa na kuaribu kabisa utamaduni wa Mtanzania? Mimi sidhani kama ni kweli uhuru wa vyombo vya habari ni kuaribu utamaduni wanchi. Leo hii, kama viongozi wa umma tumekubali watanzania wazamishwe kwenye habari za umbeya, udaku, ngono na majungu. Tanzania leo tuna magazeti na majarida ya umbea kuliko nchi nyingine yoyote barani Africa. Utasikia Fulani kapata buzi!!!, Oho Fulani kafumaniwa magomeni, oho kigogo (kiongozi) akutwa gesti ……n.k. Ebu jiulize kama waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari wanawatengenezea kizazi cha leo na cha kesho ufahamu gani? Waandishi na wamiliki wa majarida haya, na viongozi wetu wanatakiwa wajue kwamba anayeamua juu ya maitaji ya jamii kwenye habari ni jamii yenyewe na wala sio wao. Ukiwauliza watakwambia ni kwenda na wakati msemo unaotumika kuhalalisha mabaya kuwa mazuri, siku hizi tunavaa nguo fupi, na zisizofaa eti; tunakwenda na wakati. Je huo wakati tunaenda nao uko uchi? Au sisi tunaulazimisha uwe uchi. Zamani ndo watu waliishi utupu, sasa sisi leo tunaojidai kusonga mbele kwa kuvaa nguo nusu uchi, uku ni kurudi zamani na wakati, sio kusonga mbele au kwenda na wakati.
Kiongozi yeyote anayejijua kuwa yeye anapaswa kutumikia umma wa Taifa la Tanzania. Taifa lenye umaskini sana, Taifa ambalo watu wake ni wapole watulivu kuliko Taifa lolote barani afrika, Taifa ambalo watu wake wamezoea kuonyeshwa punda na kuambiwa ni ng’ombe; mbuzi na kuambiwa ni ngamia, watu ambao viongozi wao wamezoea kuwaambia kuwa ni wavivu wa kufikiria. Sasa ni wajibu wa kila kiongozi na mdau wa maendeleo ya Tanzania kujua kuwa ni viongozi na wale wenye mamlaka na wajibu mkubwa wa kuendeleza jamii na sio kujipatia manufaa na upendeleo. Kama kweli mtayazingatia haya niliyojaribu kuwaeleza nadhani huu utakuwa mwanzo mzuri wa “Taifa letu kuelekea kweye neema ya kila Mtanzania”.Mungu ibariki Africa,Mungu ibariki Tanzania.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home